Soundcloud

Zitto amshauri haya Rais Magufuli baada ya Tanesco kushindwa kesi ya IPTL na kuamriwa kulipa sh320b


Shirika la umeme Tanzania, Tanzania limeshindwa kesi yake dhidi ya IPTL na kuamriwa kulipa dola milioni 148.4 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 320 za Kitanzania.
tanesco
Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya inayoshughulika na migogoro ya uwezekaji, ICSID yenye makao yake mjini Washington DC, Marekani na ipo chini ya benki ya dunia.

Tanesco ilikuwa ikiwakilishwa na makampuni mawili ya wawanasheria R.K. Rweyongeza & Co. Advocates na Crax Law Partners ya Tanzania, pamoja na lile la Zurich, Kellerhals Carrard.

Pesa hizo zinatakiwa kulipwa kwa Standard Chartered Bank-Hong Kong (SCB-HK).
SCB-HK ililinunua deni la IPTL kwa punguzo la bei ya milioni 76.1 kutoka Danaharta Bankin ya Malaysia, August 2005 baada ya Danaharta kushindwa kuchukua mkopo wake kutoka kwa IPTL.


Hiyo ina maana kuwa SCB-HK imepata faida ya dola milioni 172. IPTL ilikopa dola milioni 100 mwaka 1998 kutoka kwenye kundi la benki za Malaysia ili kujenga mtambo umeme Tegeta wenye megawatt 100.
TANESCO ilifungua kesi ICSID baada ya kubaini kuwa imekuwa ikitozwa zaidi na IPTL. Kesi hiyo inahusiana na ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL iliyohusisha uchotwaji wa shilingi bilioni 306 za kitanzania.

Novemba mwaka jana, mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakati huo, Zitto Kabwe alisoma ripoti na kulithibitishia Bunge hilo kwamba viongozi na wafanyakazi wa serikali, wafanyabiashara, viongozi na taasisi za dini, mabenki na watu binafsi wanahusika kufanya katika ufisadifu.
Kufuatia Tanesco kushindwa kwenye kesi hiyo, Zitto amemtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua.
“Kwanini Rais Magufuli hafanyii kazi suala la IPTL? Matapeli hawa wataendelea kuipa hasara nchi yetu mpaka lini? Sasa mahakama ya ICSID imeamua kuwa Benki ya Standard Chartered ilipwe tshs 300bn na riba. TANESCO wanaingia Hasara hii Kwa sababu ya wizi wa Fedha za TEGETA Escrow na Rais bado anavuta miguu kuchukua hatua dhidi ya suala hili. Nini kimemkuta Rais Magufuli? Rais anataka tuamini kuwa IPTL/PAP Ni kweli waligharamia Mkutano Mkuu wa CCM uliompa yeye Uenyekiti,” ameandika Facebook.

“Tanzania hapo Ni hasara tupu 1)mmelipa matapeli Fedha zilizokuwa kwenye TEGETA escrow account. 2) mmewapa mtambo wa kuzalisha umeme matapeli hao na mnaendelea kuwalipa capacity charges mpaka sasa. 3) mnawalipa standard chartered Fedha zao Kwa mtambo ambao sio wenu na Kwa Fedha ambazo mngezitoa escrow a/c lakini sasa mtazitoa hazina,” ameongeza.

“Rais achukue hatua zifuatazo – awafikishe mahakamani watu wote waliohusika na kuitia Nchi hasara katika sakata la TEGETA Escrow – aitwae mitambo ya IPTL kisheria na kuimilikisha Kwa TANESCO – amkamate Bwana Harbinder Singh Seth na wafuasi wake wote na kuwafikisha mahakamani Kwa makosa ya utapeli, wizi, uhujumu uchumi, utakatishaji wa Fedha.”

“Benki iliyotumika kupitisha Fedha za TEGETA escrow ndio ilipe Hilo deni tunalotakiwa kulipa. Rais aamue kusimama na watanzania au kusimama na matapeli wa TEGETA escrow.”