Soundcloud

SERIKALI YAZIFUTIA USAJILI MELI ZILIZOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA

Serikali imetangaza kuzifutia usajili meli mbili zilizokamatwa zikisafirisha dawa za kulevya na silaha na kuzitaka kushusha bendera ya Tanzania.

“Tumefuta usajili wa meli hizo na kuwataka kushusha bendera yetu na wapambane na tatizo hilo wao wenyewe na sisi tutatoa ushirikiano wote utakaohitajika,” amesema Makamu wa Rais Samia Suluhu.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais, samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo, Januari 18, 2018 Ikulu, jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa  licha ya kuzifutia usajili, hatua nyingine zinaendelea ili kuwabaini wahusika halisi.

Makamu wa Rais amezitaja meli hizo kuwa ni Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa huko Jamhuri ya Dominican Desemba 27, 2017 ikiwa na shehena ya dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu 1,600, na nyingine ni  ni Andromeda yenye usajili IMO 7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kwenda nchini Libya kinyume cha sheria za Kimataifa.

Ameeleza kuwa meli hizo zilisajiliwa Tanzania kupitia taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli zote za nje.
“Wanaposajili wanajaza fomu mbili ikiwepo moja ya kiapo cha kutokujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, silaha au watu. Kwa wao kufanya hivyo wamekiuka kiapo walichoapa,” amesema Makamu wa Rais.

Ameendelea kusema kuwa baada ya tukio hilo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimwagiza kufanya kikao na Serikali ya Zanzibar, kikao ambacho kimetoka na mapendekezo kadhaa ikiwamo kuunda kamati maalum ya kupitia usajili wa meli zote pamoja na sheria za usajili na kodi.

Makamu wa Rais amesema katika kikao hicho kilichofanyika Zanzibar kilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine na  wamekubaliana kuunda kamati maalum itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kuanza mchakato wa kupitia meli zote zilizosajiliwa na zitakazosajiliwa kuona umiliki wake.

Post a Comment