Soundcloud

SIRI 3 DEREVA WA LISSU KUTIMKIA…

SIRI tatu za dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), Simon Bakari (pichani) kwenda Ubelgiji na bosi wake zimevuja.

Mbunge mmoja ndani ya chama hicho aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa chama wala familia, alisema kamati maalum inayoratibu matibabu ya Lissu iliyokutana jijini Nairobi, Kenya iliona ni vema Simon aongozane na bosi wake pamoja na mkewe mbunge huyo, Alicia kwa kuwa ndiye aliyefanya kazi kubwa ya kumuuguza akiwa Nairobi akisaidiana na Mkuu wa Idara ya Uenezi, Hemedi Ali.


Tundu Lissu (Chadema).
“Pamoja na ukweli kwamba dereva Simon alikuwa ana matatizo ya kisaikolojia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa na Lissu mkoani Dodoma
Septemba 7, mwaka jana, alijitahidi kutoa huduma zisizo za kitabibu pamoja na Hemedi (Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi, Chadema) Nairobi ndiyo maana kamati maalum ya kuratibu tiba ya mbunge huyo ikaona ni vema naye aongozane na bosi wake kwani bado anahitaji msaidizi,” alisema mbunge huyo.

USALAMA WA DEREVA
Akifafanua zaidi, alisema Simon kwenda Ulaya kutasaidia pia kuwa salama zaidi kama alivyokuwa Nairobi kwa sababu huko Ubelgiji, Chadema imewasiliana na serikali ya huko ili nako akapewe ulinzi mkali kwa sababu waliomshambulia hadi sasa chama chao hakijapata taarifa kama wamekamatwa au la.
Mbunge huyo alisema sababu ya tatu iliyomfanya dereva huyo kwenda na Lissu Ulaya ni uaminifu wake kwa bosi wake huyo.
“Unajua Simon kwa kiasi kikubwa alichangia kuokoa maisha ya Lissu kwa sababu mbalimbali ambazo zinaeleweka kabla na baada ya mashambulizi ya kutisha ya kama vita ya upande mmoja, Lissu mwenyewe ameshaeleza jinsi kijana huyo alivyo mwaminifu kwake kwani ameishi naye tangu akiwa mtoto,” alisema mbunge huyo.

Aliongeza kuwa sababu ya nne ni kwamba Ubelgiji atakutana na wataalam wengine wa saikolojia, hivyo atapata tiba kwa sababu tukio alilolishuhudia Septemba 7, mwaka jana Area D Dodoma lilikuwa siyo la kawaida.

LISSU ATATIBIWA HOSPITALI GANI?
Mbunge huyo alipoulizwa Lissu atapelekwa hospitali gani au mji gani alijibu: “Kwa sasa ni mapema mno kutaja hospitali isipokuwa atakapokuwa huko atapata ulinzi binafsi na pia tumezungumza na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya ulinzi zaidi.”

MAPAMBANO YA DEMOKRASIA
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uenezi wa Chadema, Hemedi Ali katika maelezo yake alikiri kumhudumia Lissu akiwa Nairobi wakati wa matibabu kwa miezi minne aliyolazwa na kufafanua kuwa hatua aliyofikia ni ya kushukuru kwa sababu alimpokea huku mwili wake ukiwa na shaka.
Alisema alikuwa akimhudumia Lissu huku akiwa katika darasa la kupata moyo wa ujasiri katika mapambano ya demokrasia.

“Nimempokea Lissu mwili wake ukiwa na mashaka lakini kupitia yeye nimeona miujiza ya Mungu, kipindi chote cha miezi minne nimejifunza ujasiri mkubwa katika mapambano ya haki na demokrasia,” alisema Ali.
Lissu aliondoka nchini Kenya Januari 6, mwaka huu siku ya Jumamosi iliyopita kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo inaaminika atafanyiwa matibabu ya viungo na pia kutolewa risasi moja iliyobaki kwenye nyonga yake.
Itakumbukwa kuwa akiwa Hospitali ya Dodoma alitolewa risasi nane na Hospitali ya Nairobi alitolewa risasi saba na alifanyiwa operesheni 17.

CHANZO:Global Publisher

Post a Comment