Soundcloud

Chenge na wenzake waula


BUNGE limewachagua wenyeviti wake kwa kuwarudisha waliokuwa viongozi katika kipindi cha kwanza cha uhai wa Bunge hilo la 11 ili waendelee kuongoza katika kipindi cha pili hadi 2020.
Wenyeviti hao waliorudishwa kuongoza vikao vya Bunge ni Mussa Azzan Zungu, Najma Giga na Andrew Chenge, ambao wamechaguliwa kwa kura za ndio na Bunge ili kuendelea kuongoza vikao vya Bunge katika kipindi cha pili cha uhai wa Bunge kinachoishia 2020. Akitangaza matokeo hayo bungeni jana, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alisema wenyeviti hao wamerudishwa kutokana na Kanuni za Bunge za mwaka 2016 ambazo zinawaruhusu pia kugombea tena na Kamati ya Uongozi yenye mamlaka ya kuteua wagombea ikaridhia na kuwateua tena ili waidhinishwe na Bunge.
Alisema kwa mujibu wa kanuni hizo kifungu namba 7 (2) pamoja na kifungu namba 11 (1) (a) kinaweka utaratibu wa namna ya kuwapata wenyeviti wa Bunge kwa kuchagua watatu kati ya majina sita yaliyoteuliwa na Kamati ya Uongozi. Dk Tulia pia alisema kanuni hizo zinawapa nafasi ya wenyeviti waliokuwapo kugombea tena na ikiwezekana kuchaguliwa tena, kutokana na kuridhika na utendaji wao, Kamati ya Uongozi ilipendekeza majina matatu badala ya sita ya wenyeviti waliokuwepo. Kutokana na sababu hiyo, kamati haikuona lazima kuongeza majina mengine badala yake majina matatu yamerudishwa na hivyo wabunge mipigie wamewapigia kura ya kukubali kwamba hao ndio wenyeviti wa Bunge.
Wakati huo huo, wabunge wawili, Dk Godwin Mollel wa Jimbo la Siha na Maulid Mtulia wa Kinondoni kwa tiketi ya CCM wameapa bungeni baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Februari 17, mwaka huu. Wabunge hao ambao awali walikuwa bungeni humo kwa tiketi ya Chadema, waliamua kukihama chama hicho na kujiunga na CCM na wakateuliwa na chama hicho kusimama kugombea ubunge katika majimbo waliyokuwa wakiongoza na wakashinda. Katika uchaguzi huo, wabunge wote wawili waliibuka washindi na hivyo wamerudi bungeni na hivyo wanatakiwa kuapa kabla ya kuanza kushiriki vikao vya bunge la 11.


Bunge hilo mara baada ya kuimba wimbo wa Taifa na dua, waliitwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuingia bungeni, wakiongozwa na askari wa bunge huku wakasindikizwa na baadhi ya wabunge kwa nyimbo kwa nyimbo. Baada ya kuapa wabunge hao, walioneshwa viti vya kukaa upande ambao wabunge wa CCM wanakaa tofauti na vile walivyokuwa wakikaa awali wakati wapo upande wa upinzani. Naibu Spika, Dk Tulia wakati wa maswali na majibu aliwapa nafasi ya wabunge hao kuuliza maswali ya nyongeza katika siku yao ya kwanza wakiwa bungeni kupitia tiketi ya CCM kuhusu mtakabali wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kuhusu kuboresha miradi ya barabara katika majimbo yao na yakajibiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Josephat Kandege kwamba mkakati wa serikali ni kuhakikisha barabara nyingi zinatengenezwa.

Post a Comment