Soundcloud

Mke wa zamani wa Mandela, Winnie amefariki


Leo April 2, 2018 Winnie Mandela, mke wa zamani wa Nelson Mandela, ambaye pia alipigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini amefariki dunia akiwa na miaka 81.
Habari za kifo chake zimethibitishwa na msaidizi wake.

Winnie alizaliwa mnamo 26 October, 1936, Kama ilivyomtokea mumewe, Bi Winnie alifungwa gerezani, na hata kuwekwa katika kizuizi cha pekee yake ambacho ni mojawapo ya vifungo vigumu zaidi gerezani vinavyowaathiri wafungwa kisaikolojia.
Lakini baada ya kuachiwa kwake mtindo wa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi ulianza kupata sifa mbaya hasa pale alipoonekana kuendekeza tabia ya kuwavisha tairi shingoni wale waliolengwa kwa tuhuma za usaliti na kisha kuwachoma moto.
"Kwa 'mikufu yetu' tutaikomboa nchi hii," alizoea kusema.
Mambo yalizidi kumwendea mrama kutokana na matendo ya baadhi ya walinzi wake katika kile kikundi kilijulikana kama the Mandela United Football Club.
Walipatikana kuhusika katika kitendo cha kumteka nyara na kumuua kijana mmoja mwenye umri wa miaka 14 aitwae Stompie Moeketsi -kwa tuhuma za kwamba alikuwa akitoa siri kwa maadui zao.
Japo Bi Winnie Mandela aliepuka hukumu ya kifungo jela - baadaye tume ya ukweli na maridhiano iliyoongozwa na askofu Desmond Tutu, iliyokuwa inachunguza ukweli kuhusu matendo tata katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na kutafuta maridhiano, ilimpata Bi Mandela na hatia ya kutowajibika kisiasa wala kimaadili wakati wa kitendo hicho.

Post a Comment